Thursday, January 24, 2013

Mji wa kiteknolojia kujengwa Kenya

Kenya imechukua hatua ya kwanza katika ujenzi wa kile inachotarajia utakuwa mradi mkubwa zaidi barani Afrika wa mji wa kiteknolojia (silicon Valley) au unaotegemea sana vifaa vya elektroniki katika kuendeleza teknolojia ya habari na mawasilaino ili kukuza uchumi.

Mji wa Konza
Rais Mwai Kibaki amezindua rasmi mradi huo katika eneo la Konza , mtaa mdogo Kusini mwa Nairobi, ambako mji huo mpya wa kiteknolojia utajengwa katika muda wa miaka 20 ijayo.
Mradi huu wenye thamani ya dola bilioni kumi na nne na nusu upo chini ya mpango wa wizara ya habari na mawasiliano.Iwapo utakamilika, Mji wa kiteknolojia wa Konza utajumuisha bustani, makaazi na mijengo ya kibiashara na kijamii.


Ujenzi wa mji wa Konza ni mradi katika ruwaza ya maendeleo Kenya kufikia mwaka 2030 na unalenga kuimarisha maisha kwa taifa zima na kulifanya kuwa na ushindani duniani ifikapo mwaka huo 2030.
Rais Mwai Kibaki ameeleza kuwa ujenzi wa Mji wa Konza utasaidia kubadili uchumi wa Kenya kwa ukubwa.

Mradi wa mji wa Konza unanuia kuendeleza viwanda vya huduma za teknolojia hiyo ya mawasiliano, na mfumo wa kupata biashara kutoka nchi za nje ili kutafuta utajiri wa mali na kutoa nafasi za ajira.
Mradi huu unasemekana kutoa nafasi zaidi ya laki moja za ajira ifikapo mwaka 2030 pamoja na kuendelea kudumisha ukuwaji wa pato jumla la nchi la asilimia 10 katika kipindi cha miaka kumi na nane ijayo.
Wizara ya habari na mawasiliano nchini ilipewa jukumu la kuidhinisha mradi huo kupitia makubaliano ya baraza la mawaziri lililouidhinisha miongoni mwa miradi mingine ili kukuza na kuendeleza sekta hiyo ya teknolojia ya mawasilino nchini.

Suali ambalo linasalia ni kuna umuhimu gani katika ulimwengu wa sasa ulioendelea kitenolojia kwa ujenzi wa mji huu na watu kuuhamia mji wa Konza?

No comments:

Post a Comment