Monday, February 04, 2013

JE, TUMEJIANDAA NA UVAMIZI WA WACHINA?

RAISI JAKAYA KIKWETE  AKIWA KAZUNGUKWA NA WACHINA

Ndugu zangu,
Jeshi la Wachina linakuja, wako wengi. Kwenye moja ya picha za magazetini hii leo, inamwonyesha Rais wetu akiwa amezungukwa na Wachina. Naam nadhani utakubaliana nami hata hii picha tu inatuonyesha.
Rais akiwa amevalia ' Kijamaa', lakini Wachina wamevalia ' Kibepari'.  Kiukweli China ni taifa kubwa kiuchumi. na Uchumi wake unakua kwa kasi kubwa, ni uchumi wa Kibepari.

Na idadi ya Wachina nayo ni kubwa. Ili kuweza kushindana kibiashara, China kwa sasa inahitaji mali ghafi nyingi kwa viwanda vyake. China inahitaji nishati pia; mafuta na gesi.Wachina wameigeukia Afrika. Wachina leo, kwa kutumia mahusiano mazuri na ya kirafiki ya kihistoria, ya tangu ya enzi za Vita Baridi vya Dunia, wanajipenyeza kila kwenye uwezekano wa kuvuna mali ghafi ikiwamo mafuta na gesi.Nao wanakuja na ahadi za misaada ikiwamo kutujengea WaAfrika barabara, viwanja vya michezo vya kisasa na hata kumbi za Kimataifa za mikutano.Duniani hakuna cha bure. WaChina wanavuna zaidi ya wanachotupa.Tujiulize; tunataka nini? Tuangalie pia, masharti ya misaada ya Wachina. Tuangalie vile vile mazingira ya ajira wanazokuja nazo Wachina katika kuwekeza kwao hapa kwetu.Ilivyo sasa, inatokea wawekezaji wa Kichina wanakuja nchini wakiwa na wafanyakazi wao, na wakati mwingine, hata vibarua wa kubeba zege wanatoka UChina. Hali hii haisaidii kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu.Na hata inapotokea Wachina wakatoa ajira, basi, mazingira ya ajira huwa magumu kwa vijana wetu. Ujira ni mdogo na masharti ya kazi kwa vijana wetu huwa magumu sana.Tujiulize pia, uwekezaji wa Wachina unatoa fursa kwa Watanzania kupata maarifa ya kiufundi na kiutawala kwenye sekta ambazo Wachina hao wanawekeza hapa nchini?Hofu yetu, kama nchi, ni kuendelea kuwa tegemezi, hivyo masikini, huku nchi yetu ikiwa na rasilimali nyingi.Na tujiahadhari, na ‘Uvamizi wa Wachina.’ Yumkinini umetukuta tukiwa hatujajiandaa, kama taifa.
 

Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment