Friday, March 15, 2013

HATIMAYE YULE POLISI ALIYEMUUA MWALIMU KWA RISASI AMEFUKUZWA KAZI


JESHI la Polisi mkoani Njombe, limemfukuza kazi askari wake PC Gelvas Joseph, mwenye namba 9790, kwa kosa la kufanya mauaji ya mwalimu wa Shule ya Sekondari Kitulo, wilayani Makete.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Focus Malengo, alisema askari huyo alifanya kosa hilo Februari 27 mwaka huu kwa kumpiga risasi kifuani mwalimu  Castory Sote (31), na kusababisha kifo chake papo hapo.

Alisema askari huyo amefukuzwa kazi baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika na kubaini alikiuka kanuni za utumishi ambapo hivi sasa anakabiliwa na mashtaka.

Aliongeza kuwa, kosa hilo alilifanya akiwa lindoni kwenye Benki ya NMB, tawi la Makete, ambapo marehemu alikuwa akichukua fedha katika mashine za benki hiyo.

Ilidaiwa kuwa, siku ya tukio hilo kulitokea malumbano kati ya mwalimu huyo na askari ambaye alimtuhumu marehemu kuendesha pikipiki bila kuvaa kofia ngumu (helmet) kichwani. Hali hiyo ilizua mzozo kati yao baada ya marehemu kudai kuwa, polisi huyo si askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

No comments:

Post a Comment