Monday, April 08, 2013

AIBU YA MAHAKAMA WILAYA YA BAGAMOYO

Umewahi kuingia ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo? Binafsi kwa mara ya kwanza niliingia Jumatano iliyopita, nikifuatilia kesi, kama ijulikanavyo kazi za waandishi wa habari.


Nikiwa ndani ya ukumbi wa mahakama ya wazi, sikuamini nilichokishuhudia katika mji huo maarufu wa kihistoria, kitaifa na kimataifa; ikiwa ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuwa mzaliwa wa wilaya hiyo.

Hata Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa ni mbunge wa jimbo hilo lenye vivutio vingi vya kihistoria.

Macho yangu yakatua katika paa la mahakama hiyo na kupokelewa na mabati yaliyotoboka-toboka, ilhali nyaya za umeme zikiwa zimetandazwa kupitia baadhi ya nguzo kwa minajili ya kusambaza umeme ndani ya jengo hilo.

Nikarejesha fikra zangu kwenye tukio la kuporomoka jengo lililokuwa na ghorofa 16 hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Nikaanza kuingiwa hofu kutokana na baadhi ya kuta kusheheni viraka huku nyufa nyingine zikishindikana kudhibitiwa na viraka, hali iliyosababisha kuta kuwa na michirizi na hivyo kutoa taswira ya uchakavu wa jengo hilo.

Nikabadili uelekeo. Nikayaelekeza macho upande wa kushoto kwangu, pembezoni mwa vizimba, jirani na mlango unaotumiwa na hakimu kuingia mahakamani. Nikahisi kuishiwa nguvu baada ya kuona majalada yakiwa yamehifadhiwa katika eneo lisilo na mlango wala dirisha.

Panapotakiwa kuwa na dirisha, pamewekwa mbao laini na kufunikwa kwa mapazia. Ikumbukwe hata kama majalada hayo ni ya kesi zilizoisha, haimaanishi kumbukumbu zake hazina maana.

Nikainamisha uso nikiwaza jinsi ya kutumia kalamu yangu angalau kutimiza wajibu wangu juu ya suala hili, macho yangu yakakutana na sakafu iliyochoka, ikiwa na nyufa za kutosha.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi, mahakama ni muhimili wa dola ambao ngazi yake ya wilaya ina hadhi ya kupokea kesi za mauaji yaliyo kwenye hatua za awali, wakili kutekeleza baadhi ya majukumu yao kushughulikia mashauri ya madai, yenye thamani ya kuanzia Sh10 mil mpaka Sh100mil.

Katika hali ya kawaida, ilitarajiwa jengo linalotumika kwa shughuli za mahakama, liwe na hadhi inayoshabihiana na umuhimu, unyeti na usiri wake achilia mbali hadhi ya utu wa mtumishi wa umma.

Kwanini hali inakuwa hivi?

Gazeti hili lililazimika kuhojiana na uongozi kwa lengo la kujua kulikoni.Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Liad Chamshama anasema “Mahakama imekuwa moja ya waathirika wa mfumo wa mgawanyo wa rasirimali za nchi usiozingatia usawa, ukiwa makini utabaini serikali kuu inapendelewa zaidi ikifuatiwa na wanasiasa.”

chanzo Mwananch

No comments:

Post a Comment