Friday, April 05, 2013


SIRI KUUAWAWA KWA ZITTO KABWE YAFICHUKA. YADAIWA ILIPANGWA ANYWESHWE SUMU HOTELINI, DK SLAA ATAJWA KUMTUMA SAANANE KUMMALIZA, MWENYEWE AKANUSHA, ASEMA NI SIASA CHAFUTISHIO la kuuawa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, sasa limechukua sura mpya, baada ya kuibuika kwa madai mapya kuwa Bosi wake, Dk. Willbrod Slaa, alipanga njama za kumuangamiza, MTANZANIA Jumatano linaripoti.

Duru za habari zinaeleza kuwa Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni, anadaiwa alitaka kuuawa kwa sumu na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Slaa, ambaye alimtumia kada na Mjumbe wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), Ben Saanane, kutekeleza mpango huo.

Habari zinadai kuwa tukio hilo lilipangwa kutekelezwa Mei mwaka jana, katika Hoteli ya Lunch Time, iliyoko Mabibo External, jijini Dar es Salaam.

Kwamba Zitto alilengwa kuuawa kwa kuwekewa sumu kwenye kinywaji chake wakati akiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya makada vijana wa chama hicho katika Hoteli ya Lunch Time.

Mmoja wa watu waliokuwa katika tukio hilo amelieleza MTANZANIA Jumatano kuwa Zitto alinusurika baada ya aliyetumwa kumuwekea sumu hiyo kuidondosha na hivyo kuonekana kwa watu waliokuwa eneo hilo.

Anamtaja mtu aliyetumwa kumuua Zitto kuwa ni Ben Saanane, ambaye aliangusha karatasi ya nailoni iliyokuwa na ungaunga unaosadikiwa kuwa sumu na kuonekana kwa watu waliokuwa eneo hilo, akiwemo Zitto mwenyewe pamoja na aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano, Shonza alikiri kutokea kwa tukio hilo kwa kueleza kuwa yeye na Mwampamba walihoji kilichokuwa ndani ya nailoni ile, ambacho kilionekana wazi kuwa ni unga unga ni nini, ambapo Saanane alikiri kuwa ilikuwa sumu ambayo alipewa na Dk. Slaa, ili amuwekee Zitto.

Shonza alidai kuwa siku ya tukio, yeye na Zitto walikuwa wamekaa meza moja na Saanane ambaye mkono wake wa kushoto ulikuwa umefungwa bandeji aliyowaeleza kuwa aliifunga kutokana na maumivu ya mkono.

Alisema wakiwa katika maongezi, huku Saanane akionyesha kuzidiwa na kilevi alichokuwa amekunywa, alitoa bahasha ya kaki yenye fedha ili alipie gharama za vinywaji vya wote ambayo ilidondoka na ndani yake ikatoka karatasi ndogo ya nailoni ikiwa na unga mwekundu.

Kwa mujibu wa Shonza, Saanane alipobanwa aeleze unga ule ulikuwa nini, awali alidai ni kilevi aina ya kuberi, huku akiwataka wasiifungue nailoni hiyo, jambo ambalo Mwampamba alilikataa na kulazimisha ifunguliwe pale pale.

“Kwa hasira Ben alitaka arudishiwe ile karatasi, lakini, Mwampamba aliondoka nayo, usiku huo huo Saanane alimtafuta Mwampamba hadi nyumbani kwake akidai apewe mzigo wake.

“Mwampamba alimwambia atampa mzigo wake kwa sharti moja tu la kusema ukweli kuhusu kilichomo ndani ya nailoni hiyo na hapo ndipo Ben alipokiri kuwa alipewa mzigo huo ambao una unga unga wenye sumu na Dk. Slaa, ili amuwekee Zitto kwa sababu amekuwa akimsakama ndani ya vikao vya chama.

“Huo ndiyo ukweli ambao nitausema popote, sasa kama Ben alitudanganya kwa kumsingizia Dk. Slaa hiyo ni juu yao wenyewe,” alisema Shonza.

Shonza alisema hali hiyo iliwaogofya na kuanza kuwa makini katika mapito yao na kuongeza kuwa Zitto bado yuko Chadema kwa sababu ana roho ngumu, mvumilivu na mkomavu wa kisiasa, anayeweza kukabiliana na mambo ya hatari.

Dk. Slaa alipoulizwa na MTANZANIA Jumatano kuhusu madai hayo, alisema hilo ni kosa la jinai, ambalo kama anatuhumiwa kulifanya anapaswa kushtakiwa kwenye vyombo vya dola badala ya tarifa hizo kupelekwa katika vyombo vya habari.

“Usipende kutumiwa na watu, lakini aliyekutuma anajua amekutuma kwa sababu gani. Sasa nitakujibu, hivi suala la kuua si ni jinai? Sasa suala la jinai linapelekwa kwenye vyombo vya dola au kwenye vyombo vya habari ?.

Huyo aliyesema yuko Chadema au yuko wapi? Aliyesema hakwenda polisi ?.

Aliyetaka kuuawa hakwenda pia? Sasa ninyi media mmekuwa nani?

“Wa kumuuliza suala hili ni Saanane mwenyewe au Shonza, wangekuwa na nia njema wangekwenda polisi au Zitto mwenyewe angekwenda polisi kushitaki kwa kutaka kuuawa,” alisema Dk. Slaa.

Naye Saanane ambaye amefanya mahojiano na MTANZANIA Jumatano kuhusiana na mambo mbalimbali mabaya ambayo yamekuwa yakielekezwa kwake, akizungumzia madai hayo alisema madai hayo hayana ukweli wowote, bali yanaibuliwa sasa na mahasimu wake kisiasa kwa lengo la kutaka kumshusha baada ya majaribio mengi dhidi yake kushindwa.

“Kwanza siku ambayo wanasema tulikuwa wote mimi sikuwa huko, nashangaa na haiingii akilini kwamba mimi niende hadi Temeke (kwa Mwampamba) tena usiku wa manane kwa ajili ya kufuata sumu ya kuulia panya.

“Hizi ndizo siasa halisi za maji taka, kuliko nipange njama za kuua mtu kwa malengo ya kisiasa, ni bora niache siasa.

Ni mwendawazimu pekee atakayeweza kuamini tetesi hizi za ovyo kabisa zinazofanywa na vijana walioshindwa kujenga hoja za maana kwenye majukwaa,” alisema Saanane.

Aliwaonya watu wanaohasimiana naye kisiasa kuacha kumchafua Dk. Slaa kwa kutumia jina lake katika mambo wanayomtuhumu, kwa kile alichoeleza kuwa ni dhambi kubwa kutunga uongo na kuusambaza ili kutafuta huruma ya umma wa Watanzania.

“Nadhani lengo lao hapa ni kumchafua Dk. Slaa kwa tuhuma hizi za uongo zilizotolewa kwa mara ya kwanza na vijana waliotimuliwa Chadema kwa kukisaliti chama na baadaye kuhongwa na makada na viongozi wa CCM ambao wamejiunga nao sasa.

“Sasa kwa tuhuma hizo, kwa nini wasiripoti polisi, inaingiaje akilini mtu kupanga njama kubwa kiasi hicho halafu ukae kimya tu,” alisema Saanane.

CHANZO: http://www.mtanzania.co.tz

No comments:

Post a Comment