Tuesday, June 25, 2013

AFYA YA MANDELA YAZIDI KUDORORA, IKULU KWA ZUMA HAKUKALILIKI..!!

Nelson Mandela ‘Madiba’.
Habari hizo ambazo awali zilifanywa siri kabla ya kuvuja wikiendi iliyopita, zinasema kuwa Ikulu ya Afrika Kusini ilikosa umakini, hivyo ikaacha gari bovu limbembe Mzee Mandela na matokeo yake lilizimika kwenye barabara kuu (high way).
Kuzimika kwa gari hilo, kulisababisha hekaheka lakini ufumbuzi wa haraka ulikosekana mpaka dakika 40 baadaye ndipo ‘ambulance’ nyingine ilipofika eneo la tukio, ikambeba Mzee Mandela na kumuwahisha hospitali.
Ikulu ya Afrika Kusini imelazimika kutoa tamko, baada ya wachambuzi kuelezea tukio hilo kwamba zilikuwa dakika 40 za hatari za Mzee Mandela, kwa maana nusura zichukue uhai wa kiongozi huyo aliyeongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, miaka ya 1900 nchini humo.
Tukio lenyewe, lilijiri Juni 8, mwaka huu (zaidi ya wiki mbili zilizopita) lakini ikawa kimya katika vyombo vya habari, japo minong’ono iliendelea kushamiri, kabla ya mambo kuwekwa hadharani wikiendi iliyopita.

KIVIPI DAKIKA 40 ZA HATARI?
Kwa mujibu wa habari pamoja na makala za wachambuzi mbalimbali wa kisiasa nchini Afrika Kusini, muda mfupi baada ya Mzee Mandela kuondolewa barabarani pale gari lilipomzimikia na kuwahishwa katika Hospitali ya Mediclinic Heart, Pretoria, uvumi ulienea kuwa ameshafariki dunia.
Mchambuzi wa siasa za Afrika Kusini, Olwethu Sipuka ambaye makala zake hupatikana zaidi kwenye Tovuti ya Politicweb ya nchini humo, alieleza kuwa zile dakika 40 zilikuwa za hatari mno kwa Mzee Mandela ndiyo maana wananchi waliamini uvumi kuwa alifia pale.
“Afadhali taarifa za gari lililomzimikia zilisambaa baadaye, kama zingewahi, wananchi wangekusanyika eneo la tukio na pengine ingekuwa hatari sana kwa afya ya Madiba,” aliandika Sipuka na kuongeza:
“Kama wananchi wangewahi kufika pale barabarani, pengine wangetaka kumbemba Madiba wampeleke hospitali. Kama wangeamini amekufa, isingekuwa rahisi kwao kukubali ambulance nyingine imbembe. Hiyo ni hatari ambayo ingeweza kumsababishia kifo.”
Kwa upande mwingine, habari zinasema kuwa baada ya gari kuzimika, Mzee Mandela hakupata huduma yoyote kwa muda wote wa dakika 40 ambazo alikwama pale barabarani.
Dk. Mamphela Ramphele ambaye naye ni mchambuzi wa siasa za nchi hiyo, alihoji katika makala yake ni kwa nini baada ya kuzimika ambulance ambayo ni ya kijeshi, haikwenda nyingine ya serikali kumchukua Mzee Mandela, badala yake ikaenda ya kiraia?
Aliandika kuwa afya ya Mzee Mandela haipaswi kufanyiwa mchezo, kwani jeshi la Afrika Kusini halina ambulance moja, ile ya kiraia haiwezi kuwa na ubora unaotoa huduma kwa mgonjwa anayestahili matibabu ya ICU (kiwango cha uangalizi wa hali ya juu).
Zipo taarifa zinazosema kuwa zile dakika 40 alizokwama barabarani, zilisababisha hali ya Mzee Mandela iwe mbaya zaidi, kwani baada ya ambulance ya pili kuwasili, aliwekwa katika mashine ya oksijeni ambayo ilimsaidia kupumua mpaka alipofikishwa hospitali.
Mchambuzi mwingine, Blade Nzimande, aliandika kuwa kutoka Johannesburg, nyumbani kwa Mzee Mandela mpaka Pretoria kwenye Hospitali ya Mediclinic Heart, ni umbali wa zaidi ya maili 31 (kilometa 50) hivyo ilihitajika umakini wa hali ya juu.
“Alitolewa nyumbani akiwa na hali mbaya, inafahamika macho yote ya wananchi wa Afrika Kusini yanafuatilia mwenendo wa afya yake. Gari lililombemba halikutakiwa kuwa na hitilafu ya injini. Kuna uzembe mkubwa umefanyika.”     

IKULU YATOA TAMKO
Kutokana na kuenea kwa uvumi huo, Ikulu ya Afrika Kusini, wikiendi iliyopita, ilitoa tamko kuhusiana na tukio hilo la ambulance iliyokuwa imembeba Mzee Mandela kuzimika barabarani.
Msemaji wa Ikulu ya Afrika Kusini, Mac Maharaj, alisema kuwa ni kweli kwamba gari lililokuwa limembeba Mzee Mandela lilizimika barabarani lakini halikumwathiri kwa chochote.
“Alikuwa na madaktari ambao walijiridhisha kwamba hakutakuwa na hatari yoyote katika kusubiri gari lingine la kumpeleka hospitali,” alisema Maharaj kwa niaba ya Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.
Aliongeza: “Ambulance iliyokuwa imembeba ilikuwa inasindikizwa na magari mengine, kwa hiyo kama hali ingekuwa mbaya zaidi, angehamishwa katika gari lingine na kukimbizwa hospitali. Haikuonekana hatari kubwa.
“Timu ya madaktari kutoka idara ya ulinzi ilijiridhisha kwamba afya ya Mzee Mandela itakuwa salama ndiyo maana waliruhusu subira hiyo ya dakika 40. Ile ambulance ni ya jeshi, tulipewa taarifa baada ya kuzimika, tukafanya juu chini kupata nyingine, ikaonekana itachelewa zaidi ndiyo maana ikatumika ya kiraia.
“Tunapenda wananchi wote wajue kuwa tupo makini na afya ya mzee wetu. Ile ambulance ya kijeshi ina vifaa vyote ya ICU na madaktari waliokuwa wamemzunguka ni madaktari bingwa, kwa hiyo wana uwezo mkubwa. Hakukuwa na uzembe hata kidogo.”

ZUMA IKULU HAPAKALIKI
Kwa mujibu wa taarifa za Ikulu ya Afrika Kusini, afya ya Mzee Mandela, inasababisha Rais Zuma asiwe na utulivu, kwani muda mwingine anafuatilia maendeleo ya kiongozi huyo aliyewahi kufungwa jela miaka 27, kipindi anaongoza harakati za kupinga sera za ubaguzi wa rangi nchini humo.
Imeelezwa kuwa tangu Aprili 29, mwaka huu, pale Zuma alipomtembelea Mzee Mandela na kuona ukweli jinsi afya yake inavyobadilika na kuwa mbaya zaidi, amekuwa hakai akatulia ikulu, badala yake hutumia muda mwingi kufuatilia maendeleo ya rais huyo wa kwanza Mwafrika nchini Afrika Kusini.
Habari zinafafanua kuwa siku hiyo, Zuma ambaye aliongozana na viongozi wengine wa Chama cha African National Congress (ANC), kwenda kumjulia hali hali, alishtushwa kuona Mzee Mandela akiwa hatikisi kichwa wala kupepesa macho.
Chanzo kimoja kutoka Ikulu ya Afrika Kusini ambacho hakikutajwa jina, kilieleza kwamba hata safari za nje, Zuma amezipunguza kwa hoja kwamba taifa halitamwelewa yeye kuwa mbali katika kipindi hiki ambacho Mzee Mandela anaumwa sana, japo afya yake inaelezwa kuimarika.

MBEKI AWATOA HOFU WANANCHI
Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amewatoa hofu wananchi wa nchi hiyo kuwa Mzee Mandela anaendelea vizuri, ingawa katika siku za hivi karibuni amekuwa akipelekwa hospitali mara kwa mara kwa ajili ya kutibiwa.
Mbeki aliyemrithi Mandela mwaka 1999, alisema kuwa ni vizuri wananchi wakadumisha sala kwa kumwombea mzee huyo badala ya kukata tamaa na kuamini uvumi kwamba ameshafariki dunia.

ANC YATAKA MANDELA AHESHIMIWE
Chama cha ANC, Jumamosi iliyopita, kilitoa tamko kuwa Mzee Mandela inabidi aheshimiwe na kwamba siyo kila mtu anaweza kuwa msemaji wa maendeleo ya afya yake.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Ikulu ya Afrika Kusini inabidi ifanye kazi vizuri kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za kweli na zenye uhakika kuhusu kiongozi huyo aliyeiongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1994 mpaka 1999.
“Chama chetu cha The African National Congress kwa mara nyingine kinataka pande zinazohusika zifanye kazi yake. Vilevile tunataka vyombo vya habari na familia, kuheshimu taarifa za faragha kuhusu Mandela.”

TATIZO NI MAPAFU
Mzee Mandela ambaye mwezi ujao anatarajiwa kutimiza umri wa miaka 95, kwa muda mrefu sasa anasumbuliwa na tatizo la mapafu kujaa maji.
Habari zinasema kuwa tatizo la mapafu, ni matokeo ya athari alizozipata akiwa gerezani kipindi alipofungwa miaka 27 jela katika miaka ya 1900.

TUMUOMBEE MZEE MANDELA
Mandela amekuwa kielelezo chema siyo tu kwa Afrika Kusini, bali Afrika na duniani kote. Nasi Watanzania kila mtu kwa imani yake ni vema kumuombea salama ili Mungu ampe nafuu na kumponya maradhi yanayomsibu kwa sasa.

No comments:

Post a Comment