Tuesday, July 02, 2013

TANZANIA YAUMBULIWA....GAZETI MAARUFU LA MAREKANI LAANIKA UKATILI UNAOTENDEKA NCHINI

 Tanzania imekosolewa  na  gazeti  maarufu  la  Marekani  wakati Rais Obama akipokewa kwa nderemo na  vifijo.

Gazeti hilo  maarufu nchini Marekani la The New York Times, limechapisha habari za kuonesha matukio ya ukatili yanayofanyika Tanzania.

 Habari hiyo iliyochapishwa katika toleo lake ya Juni 30, imeleza tukio la kuteswa na kuumiza kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka.

Mwandishi wa habari hiyo amejaribu kunukuu kauli ya Dk. Ulimboka akieleza jinsi alivyotekwa na kuteswa kinyama kisha kutupwa kwenye Msitu wa Mabwepande.

Mwandishi  huyo  amesema kuwa Tanzania inaheshimika nje ya nchi kama kisiwa cha amani ndani ya ukanda wenye machafuko wa Afrika  Mashariki.

Kwamba kutokana na sifa hizo, Tanzania imejizolea sifa na ufadhili wa fedha kutoka kwa mataifa mbalimbali yaliyoendelea, ikiwamo Marekani, ambayo mwaka jana
iliipatia zaidi ya dola milioni 480.


Alisema kuwa wakati Rais Obama akiwasili Tanzania makundi ya kutetea haki za binadamu na chama kikuu cha upinzani wanasema matukio ya vitisho na ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa yanashika kasi. “Kuna woga, si amani”.

Ananukuu kuwa waandishi wamekuwa wakishambuliwa na
mmoja aliuawa akiwa anatekeleza kazi yake ya uandishi wa habari.


Aliongeza kuwa Julai mwaka jana, serikali ililifungia gazeti huru la uchunguzi la kila wiki la Mwanahalisi, ambalo lilikuwa likiandika kwa undani kuhusu tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka, ambalo lilihusisha uhalifu huo na serikali ya Rais Kikwete.

Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari yenye makao makuu yake New York nchini Marekani, wiki jana ilimtaka Rais Obama kuliibua suala la uhuru wa vyombo vya habari atakapokutana na Rais Kikwete jijini Dar es Salaam.

Gazeti hilo pia limetaja vurugu za kisiasa kuwa zilichukua sura mpya na ambayo haikutegemewa wakati bomu la kurushwa kwa mkono lilipolipuliwa katika mkutano wa
hadhara wa kampeni za uchaguzi wa madiwani wa
CHADEMA na kusababisha vifo vya watu wanne mkoani Arusha.


Source: New York times
http://nytimes.com/2013/07/01/world/...can-haven.html 

No comments:

Post a Comment