Tuesday, July 02, 2013

WA SOUTH AFRICA NA WAGENI WAZIDI KUMUOMBEA MANDELAHALI ya ukimya sasa imetawala makazi ya Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela yaliyoko Orlando West, Soweto na yale yaliyo Jijini Johannesburg, barabara ya 12 Mtaa wa Nne, baada ya kuwa katika hekaheka kwa kipindi cha takribani wiki mbili zilizopita.

Makazi ya Mandela, yamekuwa katika hekaheka tangu alipolazwa hospitalini huko Pretoria siku 25, zilizopita akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na siku chake baadaye hali yake ikatangazwa kuwa mbaya.

Juzi na jana, mamia ya wananchi wa Afrika ya Kusini na wageni kutoka mataifa mbalimbali walikuwa wakimiminika kuzuru makazi ya Mandela huku wakiwa katika hali ya ukimya na kupiga picha za kumbukumbu wanapoweka maua na kadi za kumuombea ili afya yake iimarike.

Orlando West, Soweto

Katika makazi yake Orlando Soweto ambayo sasa yamegeuzwa kuwa eneo la makumbusho, Waafrika Kusini wengi pamoja na wageni kutoka nje, wamekuwa wakipatembelea na kutembezwa sehemu mbalimbali za nyumba hiyo na waongoza wageni.

Akizungumza na MTANZANIA, mmoja wa waongoza wageni aliyejiyambulisha kwa jina moja la Madonna, alisema hali ya wasiwasi na pilikapilika za wanandugu katika eneo hilo, imepungua jambo linalotoa fursa kwa watu kufika kuitembelea nyumba hiyo kujifunza namna Mandela alivyoishi wakati akipigania uhuru na pia kumuombea.

Alisema Waafrika Kusini wengi, wanaamini Mandela sasa amenyamaza na uamuzi wa kuamka tena akazungumza au kinyume chake iko mikononi mwa Mungu, hivyo jambo pekee muhimu kwao kwa sasa ni kumuomba Mungu atimize mapenzi yake.

Alisema, tangu aliitwa kuwa mmoja wa wafanyakazi wa kuongoza wageni katika nyumba hiyo, amekuwa akipokea wageni wengi wanaokuja kwa ajili ya kupiga picha za kumbukumbu na waafrika kusini wanaitumia fursa hiyo kumshukuru Mungu kwa kuwapatia Mandela.

“Watu wa Afrika Kusini, wameishi na Mandela kwa miaka mingi, ni baba yao, wanaamini kuwa safari yake ndefu ameisafiri salama na amewaongoza watu wake vema, wanamshukuru Mungu kwa kuwapa Nelson na sasa wanasema mapenzi yake yatimizwe. Anaweza kupumzika,” alisema Madonna.

Nje ya Nyumba hiyo, vyombo mbalimbali vya habari duniani vimepiga kambi, vikifuatilia kila hatua inayotokea hapo lakini baadhi ya wakazi wa hapa, licha ya kuwa katika hali ya utulivu wanavitimzana kwa jicho baya kwa kile wanachoeleza kuwa vinasubiri kutangazwa kwa taarifa za huzuni dhidi ya taifa hilo ili vipate kazi ya kufanya.

Mmoja wa watu waliyezungumza na gazeti, Stulla Boboo na kuonyesha kutofurahishwa na wingi wa vyombo vya habari katika eneo hilo, alisema ingawa Mandela ni mtu maarufu duniani, si jambo sahihi kwa waandishi wa habari kulizunguka nyumba yake masaa yote kwa sababu hilo linaonyesha kuwa wanachosubili ni kutangazwa kwa taarifa mbaya ili wapate cha kuitangizia dunia.

Katika makazi yake yaliyoko jijini Johannesburg, barabara ya 12, Mtaa wa Nne, ambako gazeti hili, juzi na jana lilijaribu bila mafanikio kuwapata ndugu wa karibu wa Mandela ili kuzungumzia mwenendo wa afya yake, nako lilishuhudia watu wengi wakifika kwa makundi na kuweka maua kadi za kumtakia nje ya nyumba.

Nyumba hiyo, ambayo Mandela na mkewe Graca Machel walikuwa wakiishi kabla ya kukimbizwa hospitalini mapema mwezi uliopita, sasa haina mtu zaidi ya walinzi ambao wamekuwa wakitaka wanaotaka kukutana wanafamilia kuwafuata kijijini Qunu.

“Familia ya Mandela iko kimya kijijini Qunu, lakini siku chache zijazo itakaporejea kutoka huko, itaeleza kitu ambacho watu wengi wa Afrika Kusini na dunia kwa ujumla wana shauku ya kukisikia. Ni vizuri kuwa na subira kidogo,” alisema.

Ikiwa ni siku ya 25 leo tangu Mandela alipolazwa hospitali akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu, taarifa za kitabibu zinaeleza kuwa hali yake bado ni mbaya huku kukiwa hakuna matumaini yoyote ya kubadilika.

No comments:

Post a Comment