Thursday, August 01, 2013

LULU WA SASA SI YULE WA ZAMAN MAMA KANUMBA ASEMA YEYE NA LULU SASA NI NDUGU


KUSOTA Gereza la Segerea, Dar kwa madai ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa staa wa filamu za Kibongo, Steven Kanumba kumemfanya mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kubadilisha mtindo wa maisha na kuishangaza jamii.

Lulu wa sasa si yule wa zamani ambapo inahabarishwa kuwa ameachana na tabia za kwenda kujiachia klabu, kulewa hadi kupitiliza, kulala kwenye mageto ambapo sasa amekuwa ni mtu wa kumtukuza Mungu, muumba wa mbingu na nchi.

HULALA SAA 3:30 usiku
Kwa mujibu wa mtu wa karibu na Lulu (aliomba jina lisitajwe), tangu staa huyo atoke jela amebadilika tabia, ameacha anasa za dunia hali inayomfanya wakati mwingine alale saa 3:30 usiku au saa 4:00.

ANASOMA BIBLIA KILA SIKU
“Yaani Lulu amebadilika sana tangu alipotoka jela, anasoma Biblia kila siku, zamani hakuwa hivyo. Kuna watu wanasema bado anapenda kwenda kujiachia klabu kama zamani, si kweli jamani,” kilisema chanzo hicho.

JUMAPILI AKIKOSA KANISANI ANAKOSA AMANI
Imezidi kumiminishwa kwamba Lulu amejenga tabia ya kutokosa kwenda kanisani kila Jumapili. Japokuwa zamani alikuwa akienda lakini kwa sasa ni kama dawa, akikosa anashinda akiwa hana amani.

HAENDI MAGETO YA WENZAKE
Habari zilisema kuwa kwa sasa, Lulu amekuwa mzito kunyanyua miguu yake kwenda kwenye mageto ya wenzake kama ilivyokuwa zamani.
“Zamani Lulu alikuwa anaweza kulala nje ya kwao, hasa kwenye mageto ya rafiki zake hata wiki moja na mama yake (Lucresia Karugila) asijue alipo, siku hizi ameacha. Kama atalala nje, mama yake anajua ni wapi na lazima itakuwa sehemu yenye usalama kwa mwanaye.
NINI KILICHOMBADILISHA LULU?
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Lulu amebadilishwa tabia na mama Kanumba (Flora Mtegoa) ikidaiwa kuwa mara baada ya kutoka jela, alikwenda nyumbani kwa mama huyo, Mbezi, Dar na kumuomba msamaha ambapo mama Kanumba kama binadamu alimsamehe kwa moyo mmoja, jambo ambalo Lulu hakulitarajia.

MAMA KANUMBA ANASEMAJE?
Baada ya kuzinyaka habari hizo, mwanahabari wetu alimtafuta mama Kanumba ili kueleza ukweli kuhusu mabadiliko ya Lulu ambapo alikuwa na haya ya kusema: 
“Kwa historia aliyokuwa nayo Lulu huko nyuma ni kweli  amebadilika na mabadiliko haya yametokana na mimi.

KUMBE ALIPOTOKA JELA ALIPIGA HODI KWA MAMA KANUMBA!
“Baada ya kutoka jela tu (akiachiwa kwa dhamana) Lulu alikuja nyumbani kwangu na kuniomba msamaha kwa yaliyotokea.
“Niliamua kumsamehe kwa moyo wote, kitu ambacho hakukitegemea.
“Baada ya msamaha huo, nilimkalisha chini na kumshauri kuwa aachane na mambo ya dunia. Nilimwambia yote yaliyotokea Mungu alikuwa na makusudi maalum kwake, ndiyo maana akampitisha kwenye mapito hayo ili abadilike.
“Namshukuru Mungu, baada ya mazungumzo yale Lulu aliamua kubadilika kabisa, amekuwa mtu wa kusoma Biblia. Muda mwingi anautumia kusali. Lulu amekuwa mshauri wangu mkubwa, kila ninapokuwa na jambo linalonikwaza anatumia maneno ya Biblia kunirudisha sawa, anajua sana maneno ya Mungu kunishinda hata mimi. Familia zote mbili (na ya mama Lulu) tunamuombea aendelee hivyohivyo.”
Mama Kanumba hakuishia hapo, alisema kuwa Lulu amekuwa ni mwanaye na ndiye faraja yake kubwa japokuwa Kanumba hayupo tena lakini staa huyo anaendelea kumpenda na kumheshimu kama mama yake.

AUTAJA UNDUGU NA MAMA LULU
Mama Kanumba alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa kwa sasa yeye, mama Lulu na Lulu mwenyewe wamekuwa ndugu na hiyo yote inatokana na jinsi msanii huyo alivyomfuata baada ya kutoka jela.

WASANII BONGO MOVIES HAWAAMINI
Kufuatia mabadiliko hayo, inadaiwa kuwa baadhi ya wasanii wa filamu za Kibongo wamekuwa hawaamini kama Lulu huyu si yule wa enzi za Kanumba, huku wengine wakidai baada ya muda mfupi atarejea maishayake ya zamani.

LULU NAYE
Lulu kwa sasa anadai hataki kuongea na magazeti, lakini akizungumza kupitia Kipindi cha Take One cha Clouds TV hivi karibuni, msanii huyo alikiri kubadilika kutokana na maisha aliyoishi jela. 
Alisema kwa sasa amekuwa ni mtu wa kusali na kusoma Biblia, starehe alizokuwa akiziendekeza zamani ameziacha, jambo ambalo limeshangaza watu kwenye jamii.

No comments:

Post a Comment