Friday, September 06, 2013

BAADA YA BEEF LA CHINI CHINI HATIMAYE KIKWETE AKUTANA NA KAGAME

Rais Poul Kagame wa Rwanda na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania
HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda, jana walikutana ana kwa ana mjini Kampala nchini Uganda. Hii ni mara ya kwanza viongozi hao kukutana, baada ya kuwapo na uelewano mdogo kutokana na Rais Kikwete kumshauri Rais Kagame akutane na vikundi vya waasi vinavyopigana mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Baada ya kutolewa ushauri huo, Rais Kagame alionekana wazi kutoukubali, jambo ambalo limezua mambo mengi yakiwamo ya wafanyabiashara wa nchi yake kutangaza kutotumia Bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo yao.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam jana, ilisema viongozi hao walikutana faragha katika mazungumzo yaliyokwenda vizuri.

“Viongozi wamekutana kwa saa moja katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya mji wa Kampala.

“Katika mazungumzo hayo, wamekubaliana kuendelea kushirikiana kujenga uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo, ilisema viongozi wako nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Maziwa Makuu, ulioanza jana katika Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort.

Viongozi wengine ambao wanahudhuria mkutano huo, ni pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa ICGLR, Rais wa Sudan Kusini, Silva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).

Uhusiano huo, ulizidi kuingia doa baada ya Serikali ya Rwanda kuamua kupandisha ushuru mpya kutoka dola 152 za Marekani hadi dola 500 kwa malori ya Tanzania pekee.

Katika hali ya kushangaza, Serikali ya Rwanda ilisema ushuru huo utatumika kwa kipindi cha wiki moja, jambo ambalo halikukubalika.

Lakini Msemaji wa Umoja wa Wasafirishaji Malori Tanzania (TATOA), Elias Lukumay alisema kuna hatari kubwa ya kupoteza wateja wao kutokana na tozo mpya.

Alisema kama tozo hiyo ikiendelea kutozwa, wafanyabiashara wa malori Tanzania wataathirika kwa kuwa watalazimika kupandisha bei ya usafirishaji karibu dola 500

No comments:

Post a Comment