Thursday, September 05, 2013

JE TANZANIA NI TISHIO KWA NCHI ZA EAC KIUCHUMI-MBONA YAPIGWA VITA NA VIJEMBE NA NCHI ZINGINE?

Wiki iliyopita ulifanyika mkutano Mjini Mombasa na kuhudhuriwa na marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi na Salva Kiir wa Sudan Kusini,  lakini Rais Kikwete hakuhusishwa.

Tangu Rais Jakaya Kikwete alipotoa ushauri kwa nchi ya Rwanda kukaa na waasi wa FDLR ili wamalize migogoro yao, uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda umekuwa shakani.

Uhasama huo unatokana na Kundi la M23 linaloundwa na wapiganaji wa Kitutsi likiaminika kusaidiwa na Rwanda na linapambana na majeshi ya Serikali ya DR Congo. Hata hivyo, Rwanda inapinga kuisaidia M23.

Kumekuwa na malumbano kupitia vyombo vya habari vya nchi hizo mbili huku kila upande ukirusha vijembe vya kumponda mwenzake.

Mbali na vijembe, hivi karibuni Rwanda imejitoa na kuanza kuacha kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuingizia mizigo yake, badala yake sasa imejielekeza Mombasa nchini Kenya.

Hali hiyo inaonyesha kuiathiri Tanzania hata katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo katika mikutano ya hivi karibuni ya wakuu wa nchi hizo, Rais Kikwete hakushiriki.

Mkutano huo uliofanyika wiki iliyopita mjini Mombasa na kuhudhuriwa na marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi na Salva Kiir wa Sudan Kusini walialikwa na kutuma wajumbe wao, lakini bila kumhusisha Rais Kikwete ni moja ya dalili ya Tanzania kutengwa au kuenguliwa.

Baada ya mkutano huo, marais hao wamezindua eneo jipya la bandari ambalo litasaidia kuimarisha huduma ya kupakia na kupakua mizigo.
Serikali ya Kenya imesema ujenzi wa sehemu hiyo mpya umefanyika kwa kutumia kipato cha ndani bila msaada wowote kutoka nje.


Mkutano huo unafuatia ule wa mwezi Juni uliofanyika mjini Kampala, Uganda ambao pia Rais Kikwete hakualikwa.

Katika mkutano huo ilikubaliwa kwamba, nchi za Afrika Mashariki zipunguze gharama za usafirishaji bidhaa kwa kupanua usafiri wa reli pamoja na kuboresha huduma za bandari, hususan ile ya Mombasa sambamba na kuharakishwa ujenzi wa bandari kubwa visiwani Lamu.

Kutokana na hali hiyo, Tanzania sasa imemwomba Rais Museveni wa Uganda kuisuluhisha na Rwanda.

No comments:

Post a Comment