Thursday, September 05, 2013

JWTZ YASITISHA LIKIZO KWA WANAJESHI....YAWAITA KAMBINI KUJIIANDAA KIVITA...!!

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesitisha wapiganaji wake kwenda likizo na kuwaita waliokuwa likizo kurudi makambini. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani kabisa vya kiinteligensia vijulikanavyo kama ‘KAINZI’,  uamuzi huo umeenda sambamba na kuweka hali ya utayari wa kijeshi (military readiness) kufikia asilimia 50 ( katika hali ya utulivu na amani nchini hali ya utayari wa kijeshi huwa asilimia 25 )

Kwa mujibu wa chanzo  hicho ambacho kimekuwa kikifuatilia mwitikio wa vyombo vyetu vya usalama kufuatia kuongezeka kwa hali ya utete katika eneo la maziwa makuu,  vikosi vya jeshi nchini kufikia jana vilikuwa vimeshasomewa taarifa hiyo ya kusitisha likizo na hata pasi za kutoka makambani huku maafisa wake ambao walikuwa nje ya vituo vyao vya kazi wakitakiwa kurudi makambini. 


Uamuzi huu hata hivyo haujawa wazi kama unahusu wapiganaji wote nchini au ni wa Brigedia za Tabora au Brigedia za vikosi maalum tu.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha kuaminika Brigedia za Tembo na Kifaru (Tabora) tayari zimepewa maagizo ya kuwa katika hali ya utayari endapo watahitajika kufanya ‘movement’ yoyote ya kijeshi. 


“Unajua tangu sakata la Rwanda lianze ,  vyombo vyetu vya usalama na inteligensia vimeona kuwa kuna sababu ya msingi ya kujiweka katika hali ya utayari wa kijeshi” kilisema chanzo hicho. 

Baada  ya  kufuatilia zaidi na kwa kina habari hizi,  inaonekana kuwa kuna taarifa za kiusalama ambazo zimesababisha uamuzi huu kuchukuliwa. Pamoja na uamuzi huu , habari hizi zinadokeza pia kuwa JWTZ linaweza kuwaita baadhi ya reserve ili kuliongezea nguvu zaidi. 

Kwa kawaida kama ilivyokuwa kabla ya Vita ya Kagera baadhi ya maafisa wanaoweza kuongeza nguvu jeshini ni pamoja na wale kutoka vyombo vingine vya usalama kama Polisi, Mgambo, Magereza, n.k ambavyo vinaweza kutakiwa kutoa idadi fulani ya watu kujiunga na JWTZ.

Pamoja na maamuzi hayo,  chanzo hicho kiliarifu  kuwa hata wapiganaji wa JWTZ ambao walikuwa wanaandaliwa kwenye shughuli mbalimbali za kulinda amani nao wamesitishwa sasa hivi na wanapelekwa kwenye moja ya mikoa iliyoko mpakani kwa sababu ambazo mtoa habari wetu hakutaka kuziweka wazi.

No comments:

Post a Comment