Sunday, September 15, 2013

MFANYABIASHARA ALEX MASSAWE KUTUA NCHINI

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Alex Massawe anatarajiwa kutua nchini mwishoni mwa mwezi huu na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Tanzania. Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile, aliiambia MTANZANIA jana kuwa taratibu za kumrejesha Massawe nchini zimekamilika na hakuna vikwazo vitakavyosababisha asiletwe kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kamishna Babile alisema tuhuma zinazomkabili Massawe alizitenda akiwa katika ardhi ya Tanzania, hivyo ni lazima ajibu tuhuma hizo katika ardhi ya Tanzania na si vinginevyo.

Alisema taarifa za kupandishwa kizimbani Massawe katika Mahakama ya Dubai, hazikuwa sahihi na kusisitiza hakuna mabadiliko katika taratibu zinazofanywa kumrejesha nchini ili aweze kujibu tuhuma zake.

“Process (mchakato) unaendelea vizuri, kamwe hakuna mabadiliko wala vikwazo, katika kipindi cha mwisho wa mwezi huu, anaweza kuwa nchini.

Babile alisema Serikali ya Dubai (UAE), haiwezi kumfungulia mashitaka Massawe, kwa makosa aliyoyafanya akiwa Tanzania.

“Hawezi kuhukumiwa kule, kwa sababu hawezi kufunguliwa mashitaka Uarabuni kwa makosa aliyoyafanya Tanzania,” alisema Babile.

Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari (si MTANZANIA) viliripoti kuwa mfanyabiashara huyo amefikishwa katika mahakama ya Dubai, akikabiliwa na tuhuma za mauaji, baada ya Polisi wa Kimataifa (Interpol), kuiomba Serikali ya nchi hiyo kumkamata.

Massawe anayefanya biashara zake katika miji ya Arusha, Moshi na Dar es Salaam, alikamatwa kati ya Juni, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, akitokea Afrika Kusini.

Akiwa Dubai, Massawe alikutwa na hati za kusafiria (Passport) tatu bandia zilizokuwa na majina tofauti, wakati alama zake za vidole zikitambua jina lake halisi.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imethibitisha kuwa taratibu za kumrejesha nchini, Alex Massawe zimekamilika na kuongeza taratibu hizo zinafanywa kwa karibu sana kati ya Jeshi la Polisi.

Msemaji wa wizara hiyo, Mkumbwa Ali aliiambia MTANZANIA juzi kuwa Massawe alitiwa mbaroni baada ya kufanyika taratibu za kipolisi wa Tanzania, kuwataarifu Interpol juu ya kutafutwa kwa mtuhumiwa huyo.

“Si kwamba unaofanyika ni utaratibu wa kumrejesha kwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa au watuhumiwa, Tanzania hatuna utaratibu wa kubadilishana wafungwa na Dubai, hizi ni taratibu za kipolisi.

“Imetolewa taarifa na Polisi Tanzania kwamba, huyu ni Wanted (anatafutwa) na ikitolewa taarifa hizo mtuhumiwa anawekwa katika rekodi na kukamatwa,” alisema.

Massawe anatuhumiwa kufanya uhalifu mbalimbali, ikiwamo kughushi nyaraka mbalimbali na tayari Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini Massawe, ili kujibu mashitaka yake.

No comments:

Post a Comment