Tuesday, October 22, 2013

HIVI NDIVYO MWILI WA JULIUS NYAISANGAH 'ANCLE J' KUAGWA LEO KWENYE VIWANJA VYA LEADERS CLUB..!!

Marehemu Julius Nyaisangah (katikati) akiwa katika pozi na Meneja Mkuu wa GPL Abdallah Mrisho (kushoto)

Mwili wa mtangazaji mkongwe, Julius Masyaga Nyaisanga maarufu kama ‘Uncle J’ (53), aliyefariki dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Mazimbu mkoani Morogoro, unatarajiwa kuletwa leo jijini Dar es Salaam na baadaye kuagwa kwenye Viwanja vya Leaders’ Club.

Meneja Matangazo wa Kituo cha Abood Media, Abeid Dogoli alisema mwili wa Nyaisanga uliagwa jana jioni mjini Morogoro na leo alfajiri unasafirishwa kuja Dar es Salaam.
“Mwili wa marehemu utaagwa kesho (leo) kwenye Viwanja vya Leaders, na shughuli zitaanza saa 4 asubuhi baada ya kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili,” alisema rafiki wa karibu wa marehemu, Aboubakar Liongo.
Liongo aliyewahi kufanya kazi pamoja na Nyaisanga wakati huo ikijulikana kama Radio Tanzania (RTD) na baadaye Radio One, alisema baada ya shughuli ya kuaga, mwili wake utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere tayari kwa safari ya kwenda Mara kwa mazishi.
Mkoani Morogoro, mwili uliagwa nyumbani kwake eneo la Kihonda Viwandani, na mke wake Leah Nyaisanga alisema wamepanga kuondoka Jumanne kwenda Tarime.
Nyaisanga alifariki dunia katika Hospitali ya Mazimbu inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), siku moja baada ya kufikishwa na kulazwa kutokana na maradhi ya ugonjwa wa kisukari.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Nyaisanga.
Nyaisanga pia aliyewahi kufanya kazi Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo hivi sasa ni TBC Taifa na katika Kampuni ya IPP, ambako alikuwa Mkurugenzi wa Radio One.
 
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa kutokana na kifo cha mtangazaji maarufu na mkongwe hapa nchini katika Tasnia ya Habari hususan upande wa Utangazaji, Julius Nyaisanga kwani kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa katika Tasnia hiyo”, alisema Rais Kikwete katika salamu zake.
Nyaisanga aliyekuwa Mkurugenzi wa Radio Abood, ameacha mjane na watoto wawili wa kike, Boke na Nyange.

No comments:

Post a Comment