Tuesday, November 05, 2013

JB AWAJIBU WANAOHOJI KUHUSU UKARIBU WAKE NA WASICHANA WA BONGO MOVIES

HUWEZI kumzuia binadamu kusema lolote kupitia kuona au kusikia na ndiyo maana siku zote lawama hapewi mbuzi bali binadamu.
Kumekuwa na maneno ya chini kwa chini kwamba, nguli wa sinema za Bongo, Jacob Stephen Mbura ‘JB’ ‘ametembea’ na maua mazuri ya Bongo Movies, Aunt Ezekiel, Jennifer Kyaka ‘Odama’, Shamsa Ford na Wema Sepetu. Swali ni moja tu, kuna ukweli wowote?
Madai hayo yamekuwa yakisikika sana kiasi kwamba, mara kadhaa mapaparazi wamekuwa wakimuuliza JB ambapo kwa vyovyote vile lazima akane. Si rahisi kusema ‘ni kweli jamani’.
Baadhi ya binadamu huwa hawawezi kuishi na donge moyoni, watafanya kila njia kulifikisha katika jamii, wanapoona kitu, hasa cha siri watapenda wengine wajue kama walivyojua wao.
Hata hivyo, wakati wa kufikisha ujumbe huo hujikuta habari zinavuja na kufika kwenye vyombo vya habari.
KWA NINI AHUSISHWE?
Vigezo kama ukaribu, kushirikiana kazi mbalimbali, kuonekana pamoja sehemu tofauti na mastaa hao wa kike, kutaniana vimekuwa vikisababisha staa huyo anayewakimbiza wenzake kwa mauzo sokoni, ahusishwe nao katika uhusiano wa kimapenzi. 
Linapokuja suala la kazi, mara kadhaa tumemuona staa huyo ambaye hufurahia ukimwita Bonge la Bwana amekuwa akishirikiana kwa ukaribu na wakati mwingine picha anazopigwa akiwa na kina Aunt Ezekiel, Odama, Shamsa na Wema ndizo ambazo kwa kiasi kikubwa zimezua utata na kuwafanya watu waanze kuzitafsiri wanavyojua wao.
JB ANASEMAJE?
Katika mahojiano maalum na Amani yaliyofanyika kwa takriban saa moja Machi Mosi, mwaka huu, JB aliwapangua warembo hao mmoja baada ya mwingine na kusema hakuna hata mmoja aliyewahi kutoka naye kimapenzi.
Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa minong’ono hiyo huku akisema huwa inavuka mpaka na kumfikia mke wake. Alisema huwa inamuuma sana!
"Hawa wasanii wote ni watu ambao nafanya nao kazi za sanaa nje ya hapo hakuna chochote kinachoendelea, zaidi ya yote Odama, Shamsa na Aunt nilihusika kwa sehemu kubwa kuwafundisha sanaa na hata Wema nimetoa mchango mkubwa katika sanaa yake, wananiheshimu sana na mimi nawaheshimu pia.
“Niliwafundisha misingi ya sanaa, namna gani wanatakiwa kufanya kazi ili kuliteka soko la filamu, wakanielewa na ndiyo maana wote wamekuwa wakinithamini kama mlezi wao kisanaa,” alisema JB.
Aidha, JB alikwenda mbali zaidi na kusema, upendo wa wasanii hao kwake umekuwa mkubwa kwa suala la kibinadamu haswa wanapofanikiwa kisanaa, wanajikuta lazima wamshukuru yeye kwa kuwa aliwaonesha dira.
“Nikupe mfano mzuri. Nakumbuka Shamsa (Ford) alipojifungua mtoto wake wa kwanza kwa mzazi mwezake, Dickson mimi nilikuwa mtu wa kwanza kupigiwa simu ili kujulishwa badala ya mama yake mzazi. 
“Wananiheshimu na kunijali kwani nimewapa mwanga katika mafanikio ya kazi zao ambazo kila kukicha wananufaika na matunda ambayo pengine bila mimi wasingeweza kuyapata,” anasema JB na kuendelea:
“Siku moja nilitakiwa kwenda harusini na mke wangu, akasema hana nafasi, lakini akasema ili awe ‘komfotabo’ niende na Shamsha kama mwakilishi wangu.” (JB alitoa simu na kumpigia simu mkewe).
JB: Eeeh mama.
Mkewe: Haloo baby.
JB: Eti siku ile uliposema huendi kwenye ile harusi ulichagua niende na nani?
Mkewe: Na Shamsa. JB akakata simu huku akimwambia mwandishi: “Si umesikia mwenyewe?”
KUHUSU YANAYOSEMWA
JB hakusita kuwazungumzia wanaoeneza uvumi ambao yeye ameukanusha na kusema kamwe hawezi kumzuia mtu kuzungumza lakini ukweli utabaki palepale kwamba uhusiano wake na maua hayo mazuri ya Bongo Movies, upo kikazi na hata warembo hao wamekuwa wakimshukuru kila kukicha.
ANA MVUTO! 
Ucheshi kwa JB ni miongoni mwa vitu ambavyo vimemfanya apendwe na watu wengi. Mwenyewe hapendi kukasirika, kila wakati hupenda kucheka, kila mtu anavutiwa kuwa naye karibu kitu ambacho kwake haoni tatizo kikubwa anachokipinga ni ukaribu huo kuvuka mipaka.

NDOA YAKE IPO IMARA
Kuthibitisha kuwa yeye si mtu wa kuyumbishwa na mapenzi, Bonge la Bwana alizidi kuweka bayana kuwa yeye mume halali wa ndoa iliyodumu kwa takriban miaka 10 bila kuwa na kwaro zozote na anamshukuru Mungu katika hilo.
“Namshukuru Mungu sana, tangu mwaka 2004 nilipofunga ndoa hadi leo nipo kwenye ndoa na sijawahi kuichukia ndoa yangu katika hali yoyote ile,” alisema JB.

No comments:

Post a Comment