Thursday, November 07, 2013

WEMA SEPETU AIPASUA KATIKATI CLUB YA BONGO MOVIE BAADA YA RAY KUWAKATAZA WASANII WASIHUDHURIE MSIBA WA BABA YAKE.

Wema Sepetu

Klabu ya Bongo Movie ambayo inaundwa na baadhi ya wasanii wa filamu Swahiliwood imepasuka katikati kisa kikidaiwa kuwa ni lile tamko linalodaiwa kutolewa na mwenyekiti wa klabu hiyo, Vincent Kigosi ‘Ray’ kuwa mwanachama yeyote wa kundi hilo asitie miguu kwenye msiba wa baba mzazi wa mwenzao, Wema Sepetu, marehemu Balozi Isaac Sepetu.
Tukio hilo la katazo lilitokea wakati wa maombolezo ya kifo cha mzee Sepetu kilichotokea Oktoba 27, mwaka huu katika Hospitali ya TMJ kwa ugonjwa wa kisukari ambapo msiba ulikuwa nyumbani kwake, Sinza Mori jijini Dar es Salaam.

LAWAMA ZOTE KWA RAY
Kufuatia madai hayo, baadhi ya wasanii kutoka klabu ya Bongo Muvi (majina tunayo) wamekuwa wakitoa lawama zao kwa Ray huku wengine wakidai wamejitoa kwenye kundi hilo kwa sababu halina umoja na limejaa unafiki.
Maneno hayo yalianza kusambaa baada ya Wema kumaliza kumzika baba yake Oktoba 31, mwaka huu mjini Zanzibar.


Wema Sepetu (katikati) baada ya kuwasili Zanzibar. Kushoto ni rafiki yake Kajala Masanja.

RAY AAGIZWA AITISHE KIKAO CHA DHARURA KUMJADILI
Habari za uhakika zinasema kwamba, wasanii waliotangaza kujiengua klabuni humo wameshamuomba Ray aitishe kikao cha dharura kwa ajili ya kuzungumzia hatua yake ya kuwapiga marufuku wasanii hao kutoshiriki msiba wa mzee Sepetu huku akijua wema wa binadamu unapatikana kwenye kushiriki mazishi ya wenzake.
“Kikubwa zaidi ni kwamba, Ray wakati akisambaza zile meseji alisahau kuwa kuna siku Wema aliwahi kuwaalika wasanii wa kundi la Bongo Muvi nyumbani kwake Makumbusho (Dar) wakala na kunywa, mbona hawakugoma kwenda?” alihoji staa mmoja aliyepinga katazo la Ray.

Vincent Kigosi ‘Ray’

NJAMA ZA KUINGAMIZA KABISA BONGO MUVI ZAUNDWA CHINI KWA CHINI
Habari zaidi kutoka kwenye kundi linalodaiwa kujimega kwenye mpasuko huo zinasema kuwa kuna njama za makusudi za kuiangamiza klabu hiyo kwa kuwa mbali na mwenyekiti huyo kuwazuia wajumbe wasiende msibani kwa mzee Sepetu lakini imekuwa ikiendeshwa kitemi na kibaguzi.
Ilisemakana kuwa kuna wasanii wameifanya klabu hiyo kama yao huku wengine wakiwa hawatakiwi hata kukohoa jambo walilosema si sawasawa.
“Kwa mpasuko huu, wasanii waliochukizwa na Ray wamesema nao wao wanakazia hapahapa, Bongo Muvi lazima iangamie moja kwa moja, isiwepo tena,” alisema msanii mmoja ambaye jina lake linapanda kwa kasi.

KISINGIZIO CHA WASANII WANAFIKI CHAPINGWA
Maumivu makali zaidi yaliibuka kufuatia baadhi ya wasanii waliotaka kujifanya hawajapata meseji ya Ray ambapo walisema walishindwa kushiriki msiba huo kwa sababu walikuwa ‘shooting’.
“Kuna wasanii walishindwa kuweka wazi kwamba walipokea meseji ya katazo ya Ray, walipopigiwa simu na wenzao kuulizwa kwa nini hawaonekani msibani kwa Wema walisingizia eti wako location wanarekodi!
“Kwa akili za kawaida, mwenzenu kafiwa mnaweza kushikwa na ubize wa kurekodi filamu? Hawa ni wanafiki, walisingizia vile ili ionekane wana hudhuru,” alisema staa mwingine.

MAMA WEMA ASHTUSHWA
Akizungumza na waandishi wetu kwa mara ya kwanza baada ya kusikia mwanaye alisusiwa msiba wa baba yake, mama mzazi wa Wema, Mariam Sepetu alionesha kusikitishwa sana na kitendo hicho.
Alisema kitendo hicho kilitokea wakati ambao Wema au familia nzima ilikuwa inasaka faraja na si mfarakano kwa vile kufiwa kupo na hakuna dalili wala kujiandaa.
“Nilisikitika sana, lakini siwezi kusema mengi kwa sababu vijana wanataka mwongozo ili kwenda mbele, naamini watakaa na kuondoa tofauti zao,” alisema mama huyo mwenye mapenzi makubwa na mastaa wa filamu Bongo.

KATAZO LA RAY
LILISIMAMIA HIVI
Habari kutoka chanzo chetu makini zilidai kuwa hoja dhaifu iliyotumiwa na Ray ni kwamba Wema huwa haendi kwenye misiba ya wenzake hivyo walitaka na yeye amzike baba yake mwenyewe.

MISIBA ILIYOTOLEWA MFANO
Ulitolewa mfano msiba wa aliyekuwa staa wa filamu za Bongo, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ aliyefariki dunia Januari 2, mwaka huu ambapo Wema alishindwa kufika kwa sababu alikuwa studio akirekodi wimbo wake mpya ambao haujatoka hadi leo.

MISIBA ALIYOSHIRIKI
Ilidaiwa kuwa Wema huwa hashiriki misiba ya wenzake, ikatolewa mifano misiba miwili aliyoshriki kuwa ni marehemu Sharo Milionea (Hussein Mkiety) na (Steven) Kanumba kwa sababu alikuwa mtu wake.

ANACHOSIMAMIA WEMA
Akizungumzia tukio la kususiwa msiba wa baba yake, Wema alifunguka:
“Nimesikitishwa na kitendo hicho naamini hakikuwa cha haki, mimi nimekuwa nikihudhuria misibani kwa watu mbalimbali na si kweli kwamba niko kivyangu, nimehukumiwa bure.”

RAY AINGIA ‘PANGONI’
Juzi Jumanne, Amani lilimsaka Ray kwa njia ya simu ili aelezee ukweli wa madai hayo lakini aliingia ‘pangoni’ (hakupokea simu).
Hata hivyo, katika gazeti ndugu la hili, Ijumaa la Ijumaa, Novemba Mosi, 2013 ukurasa wa mbele ambapo kuna habari yenye kichwa; WEMA SEPETU ASUSIWA MSIBA, Ray aliulizwa kuhusu madai hayo ambapo alijibu:
“Mh! Kweli Wema haendagi kwenye misiba ya watu, hata mimi sikumuona kwa Sajuki ingawa sijui kama alionekana baadaye ila kwa sasa niko sehemu mbaya nitakupigia baadaye tuongee kwa kirefu.”
Hakupiga.

MASTAA KIDUCHU MSIBANI
Pamoja na katazo hilo la Ray, wasanii wengine waliamua kwenda msibani Sinza – Mori (Dar) na wachache sana kwenye mazishi, Zanzibar.
Baadhi ya wasanii hao ni pamoja na Kajala Masanja, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’, Jacob Stephen ‘JB’, Yobnesh Yusuph ‘Batuli’, Salum Mchoma ‘Chiki’, Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’ na Jacqueline Wolper.

WASIOFIKA MSIBANI
Wengi walimsusia msiba Wema, lakini majina makubwa zaidi wakiongozwa na Ray mwenyewe ni Single Mtambalike ‘Richie’, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’, Irene Paul, Blandina Chagula ‘Johari’, Ndumbangwe Misayo ‘Thea’ na Ruth Suka ‘Mainda’.

credit: Globalpublishers

No comments:

Post a Comment