Sunday, January 12, 2014

VIONGOZI VIGOGO NDANI YA SERIKALI YA AWAMU YA NNE WAFANYA KUFURU, WAGEUZA NYUMBA ZA SERIKALI KUWA BAR ZA KUUZA POMBE


Waziri wa Ujenzi, John Magufuli akisisitiza jambo fulani siku za hivi karibuni, yeye ndiye  mwenye dhamana na nyumba za Serikali. 

DAR ES SALAAM.

VIONGOZI wa Serikali wakiwamo mawaziri, wameingia kwenye kashfa inayowaweka katika wakati mgumu, baada ya kubadili matumizi ya nyumba za Serikali walizonunua, kinyume na mikataba inavyoeleza.Nyumba hizo ambazo zilianza kuuzwa mwaka 2002 enzi ya utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ziliuzwa kwa mawaziri, makatibu wakuu na watumishi wengine wa ngazi mbalimbali za umma.


Mikataba ya kisheria ya ununuzi wa nyumba za Serikali inaeleza kuwa, mfanyakazi wa Serikali anaponunua au kukopeshwa nyumba, hatakiwi kubadili matumizi au kuuza hadi baada ya miaka 25 kupita.


Kwa mujibu wa mkataba wa mauziano kifungu Na 9 na 10, mtumishi aliyeuziwa nyumba au mrithi wake haruhusiwi kuiuza nyumba hiyo mpaka hapo itakapotimia miaka ishirini na mitano (25), kuanzia tarehe ya hatimiliki.


Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Ujenzi, John Magufuli mwenye dhamana na nyumba za Serikali kwa muda wa miezi miwili kutoa ufafanuzi wa suala hilo bila mafanikio, huku akitoa sababu mbalimbali kwa mwandishi kukwepa kuzungumzia suala hilo.


Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson Lwenge alisema kuwa anahitaji kupata ripoti kamili kutoka kwa Wakala wa Nyumba za Serikali (TBA), ili ajionee mikataba na afahamu ni wapi ilipovunjwa.


“Serikali ina nia nzuri kabisa kuwauzia watumishi wake nyumba, lakini kama kuna mikataba inakiukwa, basi TBA inafahamu kwa kina ni kwa vipi watu hao wachukuliwe hatua,” alisema.


Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, viongozi wengi ambao nyumba zao zipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza wamezibadili matumizi na kuwa za biashara.


Kwa Jiji la Dar es Salaam baadhi ya nyumba zilizouzwa kwa vigogo hao wa Serikali na kubadilishwa matumizi zipo katika maeneo ya Oysterbay.


Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya nyumba hizo zikiwa zimebadilishwa matumizi na kuwa klabu za starehe, kupangishwa taasisi au balozi, huku nyingine zikiwa tayari zimeuzwa.


Moja ya nyumba hizo ni ya aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano, Mohamed Seif Khatib, iliyopo Oysterbay, Mtaa wa Bongoyo katika Barabara ya Hillpark. Nyumba hiyo kwa sasa imevunjwa na kujengwa klabu na baa iitwayo Ocasa.


Alipoulizwa kuhusu nyumba hiyo na mkataba wake unavyosema, Khatib alisema kwamba hajavunja sheria yoyote kwa sababu hajauza nyumba hiyo.


MWANANCHI

No comments:

Post a Comment