Monday, February 17, 2014

WASTARA APATA AJALI TENA

MAJANGA! Siku chache baada ya hivi karibuni kudaiwa kunywa sumu, staa mkubwa wa sinema Bongo, Wastara Juma amepata tena ajali mbaya.
Wastara Juma.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti namba wani la burudani Bongo, Ijumaa Wikienda mwishoni mwa wiki iliyopita zilieleza kuwa siku ya tukio Wastara alitoka nyumbani kwake Tabata-Bima, Dar na gari lake aina ya Toyota Vitz kwa ajili ya kwenda kununua umeme.
Akizungumzia tukio hilo kwa masikitiko, Wastara aliliambia gazeti hili kuwa kabla ya kufika kwenye kituo cha kununulia umeme (Luku) alikutana na lori kubwa lililokuwa kwenye mwendo kasi huku likiwa limewasha taa fulu.
Gari aina ya Toyota Vitz alilopata nalo ajali Wastara.
Alisema kuwa alijaribu kulikwepa lakini lilimsukuma na kujikuta akiingia mtaroni kutokana na barabara kuwa nyembamba ambapo aliumia sehemu za kichwani na mguuni kwa ndani.
Wastara alisema baada ya hapo alikimbizwa katika Hospitali ya TMJ, Dar ambapo alisafishwa majeraha (dressing) kisha akapatiwa matibabu na baadaye aliruhusiwa kurudi nyumbani.
“Nimenusurika kifo, namshukuru sana Mungu kwani ajali ilikuwa mbaya nilihamishwa kwenye siti niliyokuwa nimekaa na kurushwa kwenye siti nyingine huku nikijigonga na kuumia kichwani.

“Pia gari langu limeharibika sana, kioo chote kimevunjika, sielewi kwa nini haya yote yananitokea.
“Namuomba Mungu anisaidie maana naona mambo yanakwenda ndivyo sivyo na kwa nguvu zangu mwenyewe siwezi,”alisema Wastara.

Hata hivyo, Wastara kwa sasa anaendelea vizuri japokuwa bado anaumwa kichwa na mguu.
Wastara ameshapata ajali mara kadhaa ikiwemo ile ya pikipiki aliyopata mwaka 2008 akiwa na aliyekuwa mumewe, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ambapo ilibidi akatwe mguu wa kulia. Pia aliwahi kupata nyingine ya gari akiwa na Sajuki.

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Wastara, kuna watu wanamtakia mabaya ili amfuate Sajuki aliyefariki Januari 2, mwaka jana.

No comments:

Post a Comment