Wednesday, April 02, 2014

MAINDA, HEBU ONA AIBU BASI!! HII NI BARUA NZITO KWAKO

Staa wa Bongo Muvi, Ruth Suka ‘Mainda’.
KWAKO,
Ruth Suka ‘Mainda’, zamani uliitwa Mwanaidi kabla ya kungia kwenye ‘njia hii’. Ni imani yangu unaendelea vyema na shughuli zako za kila siku. Kwanza nakupa pole kwa habari iliyotoka katika gazeti damu moja na hili, Ijumaa Wikienda, toleo la Jumatatu iliyopita (achana na la juzi).
Habari hiyo ilikuwa na kichwa kinachosomeka: MADAI MAZITO... MAINDA MJAMZITO!Inawezekana habari hiyo haikukufurahisha kutokana na maneno uliyoandika kwenye mitandao ya kijamii ukikanusha vikali.
Ulichokuwa unajaribu kufanya ni kutudhalilisha sisi kama wanataaluma ya habari tuonekane ni wazushi, hatujui miiko ya kazi yetu. Nilipitia ujumbe wako mstari kwa mstari, nikagundua mahali palipokukwaza.
Lakini Mainda, hebu nikuulize kitu: kuwa na mimba ni kosa? Ni kashfa? Isitoshe, gazeti  lilieleza juu ya madai hayo na kuyafuatilia.
Habari ilizingatia kanuni zote, ikiwemo kukupa haki ya kutoa ufafanuzi. Siku kadhaa nyuma, uliwahi kueleza mwenyewe kuwa kutokana na chango lililokuwa linakusumbua, ulishauriwa kupata mimba ili uwe sawa. Hapo tulitunga sisi?
Mwisho wa waraka wako, nikapata picha ya tofauti. Hasa pale ulipokanusha kuwa eti umezushiwa kuwa uliwahi kuchoropoa mimba! Nani angejua siri zako kama usingesema?
Nafikiri tatizo siyo mimba, ila kinachoonekana kuwa tatizo kwako ni Ray (Vincent Kigosi) kuhusishwa katika habari ile. Tatizo ni nini? Si wewe mwenyewe ulisema uliwahi kutoa mimba ya Ray?
Ulizungumza mbele ya wahariri huku vyombo vya kurekodia vikiwa mbele yako, iweje leo unakanusha?
Ngoja ninukuu sehemu ya habari hiyo ambayo pengine ndiyo imekuchefua: ‘Kama kweli Mainda atakuwa mjamzito basi itakuwa ni mimba ya pili baada ya kukiri kuwa aliwahi kuchoropoa ya aliyekuwa mtu wake, mwigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’ ambaye walishamwagana’.
Kuna kosa hapo? Maana umelalamika ni kwa nini unahusishwa na mtu ambaye huna uhusiano naye. Sikia Mainda, huwezi kubadili historia. Ray ni sehemu ya historia ya maisha yako, maana umekiri mwenyewe kuwa aliwahi kuwa mpenzi wako.
Umesema mwenyewe kuwa, uliwahi kupata mimba yake, lakini baadaye ukaichomoa. Nikukumbushe? Angalia chini hapa...
Risasi: Unauzungumziaje uhusiano wako na Ray? Namaanisha ni nini hasa ambacho hakitaweza kufutika kirahisi katika kumbukumbu zako?
Mainda: Daah! (anavuta pumzi ndefu kisha anazishusha) nilimpenda sana Ray. Ilifikia hatua nikapata mimba yake. Mapenzi yetu yakaongezeka lakini kwa bahati mbaya ilitunga nje ya kizazi na ilinitesa sana, tena kwa kuwa ilikuwa ni mimba ya kwanza sikuwa nimejitambua mapema. Madaktari wakashauri niitoe, nikakubaliana nao.
Hiyo ni sehemu ya mahojiano yako na wahariri wa Global ambayo habari yake iliandikwa na Mwandishi Wetu, ikatoka katika gazeti hili ikiwa na kichwa: MAINDA: NIMETOA MIMBA YA RAY!
Nani anadanganya? Sisi au wewe? Kuwa mkweli bwana. Heshima yako kama kioo cha jamii ni kubwa. Si jambo jema kuwashushia heshima watu ambao wamechangia kukupa heshima!
Hebu ona aibu basi!
Yuleyule,
Mkweli daima,
.............................
Joseph Shaluwa.

No comments:

Post a Comment